TANAPA YASHINDA TUZO YA KIMATAIFA YA UBORA 2025 KWA MARA YA SITA MFULULIZO

Posted On: May, 31 2025
News Images

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa mara nyingine tena limeshinda tuzo ya Ubora wa Kimataifa ya mwaka 2025 – (European Award for Quality Choice Achievement 2025) katika daraja la Diamond inayotolewa na Jumuiya ya Ulaya inayojishughulisha na utafiti wa viwango vya ubora – (European Society for Quality Research ESQR).

Tuzo hii ambayo imepokelewa katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na ESQR, Stockholm, Sweden usiku wa jana tarehe 29.05.2025 na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Mussa Nasoro Kuji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Olle Meing’ataki na Afisa Uhifadhi Mkuu Eunice Msangi ambaye anasimamia Mifumo ya Usimamizi wa Ubora ya TANAPA.

Hii ni ni tuzo ya sita ya heshima ya Almasi, iliyotolewa na Jumuiya Maarufu ya Utafiti wa viwango vya Ubora ya Ulaya (ESQR) tarehe 29 Mei, 2025, inasherehekea ushindi wa sita mfululizo kwa TANAPA ikithibitisha mbinu za ubora za huduma ya utalii na juhudi katika uhifadhi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa ESQR Michael Harris alilitangaza “Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania kutunukiwa Tuzo ya Ubora wa viwango kwa 2025 kwa kutambua mchango wake wa kipekee katika uhifadhi na huduma za utalii."

“TANAPA imekuwa mshindi wa tuzo ya ubora wa juu katika uhifadhi na huduma za kiutalii” Bwana Harris alitangaza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.

Naye, Balozi wa Tanzania Nchini Sweden Mobhare Matinyi alisema kuwa

"Ni Furaha kwa Tanzania kupitia Shirika lake la TANAPA kutambuliwa kama moja ya washindi wa Tuzo ya Ubora wa ESQR mwaka 2025 kwa mwaka wa sita mfululizo. Mafanikio haya yanathibitisha Tanzania kama eneo kuu la utalii kwa jamii za kimataifa, na dunia kwa ujumla”alisema Balozi Matinyi.

Kamishina wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji alisema anaitoa tuzo hiyo maalumu kwa Rais wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake binafsi za kuitangaza Tanzania na kuwa nchi inayoshika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio bora zaidi, hata hivyo Mhe. Rais amevitangaza kupitia filamu mbili zenye thamani kubwa "Tanzania: The Royal Tour na “Amazing Tanzania".

"Rais Dk. Samia anastahili tuzo hii kutokana na sababu mbili, moja ya filamu mbili alizoshiriki maarufu zimetoa ufahamu zaidi kuhusu uzuri wa nchi duniani na mbili kwa mwongozo wake, maagizo na mchango wake katika utoaji wa huduma za hali ya juu kwa sekta ya utalii na uhifadhi nchini" alibainisha Kamishna Kuji.