TANAPA YAADHIMISHA SIKU YA ASKARI WANYAMAPORI DUNIANI KWA GWARIDE MAALUMU

TANAPA imetumia Siku akrama ya Askari Wanyamapori Duniani inayoadhimishwa Julai, 31 kila mwaka kuwaenzi na kuwakumbuka askari wake shupavu walioaga dunia uwandani wakilinda na kuwasemea kwa vitendo wanyamapori na misitu ndani ya Hifadhi za Taifa 21 zinazosimamiwa na TANAPA.
Sanjari na kuwaenzi mashujaa hao pia, imetoa tuzo kwa askari wake hodari waliookoa maisha ya askari wenzao wakati wakipambana na majangili, wanyamapori wakali, kulinda wageni na mali zao pamoja mali za shirika. Tuzo hizo ni ishara ya heshima kwa kutambua mchango mkubwa unaofanywa na askari katika kulinda tunu hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mgeni Rasmi ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Dkt. Robert Fyumagwa alisema, “Tukio la leo ni zaidi ya sherehe na ni fursa mahsusi ya kutambua mchango mkubwa wa askari wa Uhifadhi katika kulinda maliasili zetu. Maliasili hizi ni urithi wetu sote. Hivyo jukumu la kulinda hazina hii si la askari wa TANAPA tu bali jukumu la watanzania wote.“
Vilevile, Dkt. Fyumagwa aliongeza kuwa Bodi ya Wadhamini - TANAPA inatambua mchango na kazi nzuri inayotekelezwa na askari hao na kuahidi kuendelea kusimamia uboreshaji wa stahiki za askari ili wafanye kazi kwa weledi, maarifa, kujituma na kutanguliza mbele maslahi ya taasisi hiyo na taifa kwa ujumla.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi CPA Alhaj Musa Nassoro Kuji alisema, “Kutokana na kutambua mchango wa askari wetu, shirika limetoa tuzo na vyeti kwa askari 40 wa Uhifadhi kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya katika maeneo yaliyohifadhi na kusisitiza zoezi hilo litakuwa endelevu.”
Aidha katika maadhimisho hayo, TANAPA iliandaa gwaride maalumu la kuwakumbuka na kuwaenzi askari waliopoteza maisha yao kwa kuuwawa na majangili, wanyamapori, ajali, waliogongwa na nyoka sambamba na wale waliopata vilema vya kudumu wakati wakitekeleza majukumu yao.
Maadhimisho hayo pia yaliambana na onesho la shughuli za doria zilivyokuwa zikifanyika tangu mwaka 1959 wakati shirika hilo lilipoanzishwa. Kwa kipindi hicho shughuli za doria zilitumia miguu kwa asilimia 100, baadae baiskeli, pikipiki, magari aina ya Randlover (Mandolini) lakini kwa sasa vitendea kazi vimeboreshwa, kwa kuwa doria nyingi hutumia magari ya kisasa, ndege nyuki na Helkopter.
Siku ya Askari wa Wanyamapori Dunia kwa upande wa TANAPA imeadhimishwa leo Julai 31, 2025 ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire iliyopo mkoani Manyara na kuhudhuliwa na wageni mbalimbali Waandamizi kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.