ZAIDI YA WATANZANIA 230 KUADHIMISHA MIAKA 63 YA UHURU KATIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeongoza Watanzania na wapandaji wengine zaidi ya 230 kutoka mataifa ya China, Marekani na Ufaransa leo Desemba 05, 2024 kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia Lango la Marangu lililopo mkoani Kilimanjaro.
Watu hao wamepanda mlima huo kwa lengo la kwenda kupandisha Bendera ya Tanzania ikiwa ni ishara ya kumbukumbu ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wiliya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lazaro Twange, amewaasa wapandaji waliojitokeza kupanda mlima Kilimanjaro kulinda mazingira ya mlima kwa kupanda miti.
DC Twande alisema, Tunapopanda miti tutarejesha uoto wa asili, uoto ukirejea barafu itaongezeka na kusababisha ongezeko la maji yanatiririka katika mabwaya ya Nyumba ya Mungu, pangani na Lake Chala, kwani chanzo chake ni mlima Kilimanjaro.
Naye, Mwenyekitii wa Bodi ya Wadhamini TANAPA (Jenerali Mstaafu) George Waitara aliwataka wapandaji hao kuwa na uvumilivu na kusaidiana wanapoona mwenzao amekumbwa na ugonjwa wa mlima.
"Nawaasa wapandaji wote kufuata maagizo na maelekezo kutoka kwa viongozi wa mlima (guides), viongozi hawa ni wazoefu wa huu mlima na wanajua dalili zote, wakiwaambia tembeeni taratibu au kunywa maji fanyeni hivyo, mkifanya hivyo mtafika kileleni, aliongeza Jenerali Waitara.
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana Mwishawa, alishukuru kundi kubwa la Mabalozi waliojitokeza kupanda mlima na kuongeza kuwa uwepo wao sio tu ni hamasa kubwa kwa Watanzania bali pia wataendelea kuwa Mabalozi wazuri wa utalii katika nchi wanazozisimama hasa hasa kuutangaza mlima kilimanjaro na vivutio vingine kuvutia watalii wengi zaidi.
Vilevile,Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Zara Tours, kampuni aliyopewa dhamna ya kuwapandisha watu mlimani, Ndugu Bernard Sahini alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wapandaji wote usalama wa hali ya juu na huduma nzuri Kwani wamejiandaa vyema na watafanya kazi kwa weledi uliotukuka.
Hafla iyo ya kupandisha watu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika kupitia kampeni ya TWENZETU KILELENI imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, ikiweno Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali,Jeshi la Wananchi (JWTZ), Bodi ya Wadhamini TANAPA,kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali wa dini.