WAITARA AZINDUA MRADI WA MAHEMA KWA AJILI YA MALAZI HIFADHI YA TAIFA KISIWA CHA SAANANE.

Posted On: May, 26 2025
News Images

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali (mstaafu) George Waitara, amezindua huduma ya malazi ambayo ni Mahema katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane iliyopo jijini Mwanza kwa ajili ya kuvutia wageni wengi kutembelea na kupata huduma ya malazi tofauti na awali.

Hafla ya uzinduzi wa mradi huo wa mahema uliochagizwa na ongezeko la watalii uliosabababishwa na Filamu mbili za “The Royal Tour na Amazing Tanzania” na maoni ya wageni na wadau wa utalii umeziduliwa Mei 23, 2025 katika hifadhi hiyo iliyopo katikati ya jiji la Miamba.

Akizindua mahema hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali (mstaafu) George Waitara, alisema mradi huo ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya TANAPA kuboresha huduma za malazi na miundombinu mingine ya utalii katika Hifadhi za Taifa nchini.

“Mahema haya yamejengwa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kwa watalii na yatatoa huduma ambazo watalii wataridhika nazo zikiwemo sehemu za kulala zenye viwango vya juu, bafu za kisasa, na uwapo nje ya mahema hayo ukipunga hewa utaona mandhari ya kuvutia ya Ziwa Victoria,” alisema Waitara.

Aliongeza kuwa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ina mpango wa kuongeza vivutio vingine kama vile Sokwe ili kuvutia watalii wengi zaidi na mpango wa kuanzisha safari za boti kutoka Rubondo, Saanane na kufika Nyatwali iliyopo katika Ghuba ya Speke ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ajili ya kuvutia watalii wengi zaidi.

“Hifadhi yetu hii ndio Hifadhi ndogo, wanyama ni wachache lakini tutaendelea kubuni vivutio vingine vingi ili kuvutia watalii zaidi kwani Saanane imeshakuwa sehemu nzuri sana ya kupumzika.” Alisisitiza Waitara.

Aidha, Kamishna wa Uhifadhi, Hifadhi za Taifa Tanzania Musa Nassoro Kuji alimshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi za kuendeleza shughuli za Utalii kwa kuongeza miundombinu mbalimbali ndani ya Hifadhi za Taifa.

“ Ufunguzi wa mahema haya ni mkakati wa kuboresha miundombinu ya malazi kwa sehemu ambazo hazikuwa na malazi hayo hapo awali. Kama tunavyojua hifadhi hii ilikuwa na utalii wa kwenda na kurudi (day trip) sasa watalii watalala na kuongeza mapato ndani ya TANAPA na Taifa kwa ujumla.” Alisema Kuji.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Tutindaga Mwakijambile ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane alielezea Mradi huo wa mahema matatu yenye uwezo wa kulaza wageni sita (6) na watalii nane (8) kwa wageni watakaokuwa na watoto. Aidha, mradi huu pia ni moja ya maoni ya baadhi ya wageni waliotembelea Hifadhi hii pamoja na wadau wa maendeleo ya utalii.

Akizungumzia huduma ya malazi ndani ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, mmoja wa Wadau wa utalii jijini Mwanza, Benedict Charma Mongitta wa “Serengeti Services and Tours Co. Ltd” aliipongeza Serikali na TANAPA kwa ubunifu huo huku akiomba idadi ya mahema iongezeke kutoa fursa kwa wageni wengi zaidi kutalii na kulala ndani ya hifadhi.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa 21, ikiwa ndiyo inayopatikana katikati ya mji. Hifadhi hii ina vivutio mchanganyiko ikiwemo mandhari nzuri ya asili, wanyamapori, utalii wa kutembea kwa miguu, utalii wa Ziwani, michezo na uvuvi wa kitalii.