RAIS SAMIA ATOA FIDIA BILLIONI 59 KWA WAKAZI WA NYATWALI WILAYANI BUNDA

Posted On: Sep, 10 2024
News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kiasi cha Tshs. Billioni 59 kwa ajili ya zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa kata ya Nyatwali iliyopo Wilayani Bunda, Mkoani Mara.

Zoezi hilo la ulipaji fidia limeongozwa na Mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe.Dkt. Vicent Anney ambapo jumla ya wakazi 4111 wa kata ya Nyatwali leo wameanza kulipwa fidia ili kupisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ajili ya Uhifadhi na uendelezaji wa eneo hilo ambalo ni mapitio ya Wanyama hasa Tembo huku ikitaarifiwa kuwa eneo hatarishi kwa Maisha ya wananchi hao.

Akizungumza wakati wa zoezi la utoaji wa malipo Mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Anney alibainisha kuwa Mhe. Rais Samia amewatuma kumaliza hili jambo la Nyatwali na kusisitiza kumalizwa kwa migogoro ya kifamilia haraka ili wahusika wapokee malipo yao

“ Kwa ndugu zangu wenye migogoro katika maeneo na ndugu zenu malizeni migogoro kwa haraka mkishamaliza migogoro mje kwa maandishi ili muweze kupokea hundi za malipo yenu “alisema Mhe. Anney

Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Kuji aliishukuru serikali kwa kutoa fedha za kuwafidia wananchi wa Nyatwali pamoja na kupongeza umoja na mshikamano wa wananchi hao ikiwa ni pamoja na kukubali kufidiwa ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo

“Tuko kwenye zoezi muhimu sana, nimefurahi kuona wananchi wako tayari kufidiwa na wameruhusu kuachia eneo hili kutumika katika uhifadhi kwa kweli sasa hivi ikolojia ya Serengeti imerudi na hii itaongeza utalii kwa upande wa magharibi na hii itakuwa chachu ya kufikia ilani ya chama ya kuongeza watalii millioni 5 na mapato dola za kimarekani billioni 6 ifikapo 2025”

“Nimeongea na watu hapa Nyatwali wamefurahi sana na wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali, kuwasikiliza, pamoja na kuthamini kwa kuwalipa fidia zao na wako tayari kuachia eneo hili na kwenda kwenye makazi mapya na kikubwa zaidi ni kwa amani na utulivu”

Bi. Mgesi Kisuka Machiro, ambaye ni Mwananchi wa kwanza kukabidhiwa hundi ya malipo kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Nyatwali ameishukuru serikali kwa kutekeleza ahadi hiyo ya kutoa malipo hayo na kueleza kuwa sasa wanaondokana na kero za wanyama wakali na waharibifu kama Tembo, Viboko na Mamba ambao walikuwa hatarishi kwa usalama wao na hata kuathiri maendeleo ya watoto kwa kushindwa kuhudhuria masomo kwa kuongopa kupata madhila ya wanyama hao wakali.

Eneo la Nyatwali ambalo lipo magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti linatarajiwa kuwa na fursa za kitalii ambazo zitanufaisha wananchi wa wilaya ya Bunda, mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imerudisha eneo hilo kwa ajili ya kuimarisha huifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.