MAJALIWA AIPONGEZA TANAPA KWA MCHANGO MKUBWA KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII NCHINI

Na Philipo Hassan - Mwanga
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa (Mb) amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo Machi 25, 2025 katika hafla fupi ya uzinduzi wa lango jipya la utalii la Ndea lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi katika Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
“Leo tunazindua lango la Ndea kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Lango hili limejengwa kimkakati kwani lipo karibu na majirani zetu wa Hifadhi ya Tsavo iliyopo nchini Kenya ambapo ni karibu na Hifadhi ya Taifa Mkomazi hivyo, uimarishaji wa miundombinu hii ya utalii utasaidia kupokea watalii watakaotokea nchi ya Kenya na kuingia Hifadhi ya Taifa Mkomazi kujionea vivutio mbalimbali ikiwemo faru weusi.”
“Niwapongeze TANAPA kwani ninyi ni taasisi kubwa nchini katika masuala ya uhifadhi na utalii na mmekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya utalii hapa nchini. Tumeshuhudia TANAPA ikifanya maboresho makubwa kwenye sekta ya uhifadhi na utalii na matokeo yake tumeanza kuyaona yanavyonufaisha wananchi hasa waliopo karibu na maeneo ya hifadhi zetu” alisema Mhe. Majaliwa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu alieleza manufaa yatakayopatikana baada ya kuanza kutumika kwa lango hilo ikiwemo kuchangia kukuza uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Mwanga kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazotokana na mnyororo wa thamani wa biashara ya utalii itakayofanyika kupitia lango hilo.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Juma Kuji alimpongeza kwa kushiriki katika uzinduzi huo na aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekuwa chachu ya ukuaji wa maendeleo ya sekta ya Uhifadhi na Utalii nchini na kuongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo unatoa fursa zaidi za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa nchini na maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.
“TANAPA tunatoa pongezi kwako Mhe. Kasim Majaliwa, kwa kuja katika eneo la mradi na kuzindua rasmi geti hili ambalo litakuwa na faida nyingi ikiwemo kuimarisha uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Mwanga hususani waliopo katika Tarafa ya Jipe Ndea, na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hii. Pia, kwa kuwa lango hili litakuwa na miundombinu ya ulinzi wakiwemo askari na vitendea kazi vyao watasaidia kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo pamoja na kuboresha mahusiano kati ya Hifadhi na jamii” alieleza Kamishna Kuji.
Aidha, Kamishna Kuji aliongeza kuwa Serikali kupitia Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetekeleza jumla ya miradi ya kimkakati kumi na moja (11) ndani ya hifadhi hiyo na maeneo jirani huku akibainisha kuwa mradi wa ujenzi wa geti la Ndea umegharimu jumla ya shilingi za kitanzania milioni 350 na umehusisha ujenzi wa lango dogo, Ofisi, ujenzi wa choo cha wageni chenye matundu matano, ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 4.5 na uwekaji wa mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki.
Lango la Ndea lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi jirani na Kijiji cha Karambandea, katika Kata ya Toloha,Tarafa ya Jipendea Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.