KATIBU MKUU WA UN TOURISM ATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA ARUSHA

Wajumbe kutoka Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa shirika hilo, Zurab Pololikashvili, leo Aprili 24, 2025 wamefanya ziara katika Hifadhi ya Taifa Arusha iliyopo jijini Arusha, kwa lengo la kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Zurab Pololikashvili pamoja na wajumbe wengine kutoka shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) waliambatana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), ambapo walitembelea maeneo kadhaa ya kipekee ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo maporomoko ya maji ya Tululusia sambamba na kuona kwa karibu aina mbalimbali za wanyamapori wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Wajumbe hao walipokelewa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Eva Malya ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha wakishirikiana na Maafisa na Askari kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Ziara hiyo inalenga kuongezeka ushirikiano kati ya Tanzania na mashirika ya kimataifa katika kukuza utalii endelevu na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.