KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAPONGEZA JUHUDI ZA WIZARA KUPITIA TANAPA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI HIFADHINI.

Posted On: Mar, 13 2025
News Images

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa hatua kubwa walizofanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire ambayo itawezesha watalii wengi kufika kwa urahisi ndani ya hifadhi hiyo.

Kamati hiyo imetoa pongezi hizo leo Machi 12, 2025, katika ziara yake ya ukaguzi wa mradi wa Lango la kuingilia watalii la Mamire katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire pamoja na ukarabati wa barabara mbalimbali zilizoko ndani ya hifadhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava(Mb),alisema kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii na kwamba kamati yake itaendelea kufuatilia kwa karibu kasi ya utekelezaji wake.

Mnzava alisema kuwa “Tunaipongeza TANAPA kwa utekelezaji mzuri wa miradi hii, tumeridhishwa na hatua ambazo zimefikiwa na tunaamini miradi hii itakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa kwa wananchi wa wilaya ya Babati”

Aidha, Mnzava aliongeza kuwa TANAPA inapaswa kushirikiana bega kwa bega na TARURA kuhakikisha kuwa barabara inayotoka Babati hadi Lango la Mamire kuingia Hifadhi ya Taifa Tarangire inapitika vizuri ili kuongeza urahisi wa usafiri kwa wageni hatua itakayochangia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.

“Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya utalii, tunaendelea kutekeleza mikakati inayovutia watalii zaidi na kuongeza mapato ya taifa kwa njia endelevu,” alisema Kitandula.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji, alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa kwa kasi katika sekta ya utalii hivyo TANAPA itaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi wa wilaya ya Babati na kwa taifa pia.

Mradi wa ujenzi wa lango la kuingilia wageni Mamire ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire umegharimu kiasi cha shillingi Billion 3.9 ikihusisha ujenzi wa Lango, vyoo, nyumba za kulala watumishi, kisima cha maji pamoja na mifumo mbalimbali ya umeme na unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi juni, 2025.