KAMATI YA BUNGE YA PAC YAIELEKEZA TANAPA KUENDELEA KUSIMAMIA MIRADI YA MIUNDOMBINU YA UTALII HIFADHI YA TAIFA SAADANI

Posted On: Mar, 27 2025
News Images

Na: Zainabu Ally – Saadani

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa maelekezo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuendelea kusimamia miradi ya miundombinu ya utalii inayotekelezwa ndani Hifadhi ya Taifa Saadani ili kurahisisha watalii kufika kwa urahisi, kuchochea shughuli za kiutalii na kuongeza mapato ya Serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japheti Hasunga (Mb), alitoa maelekezo hayo janaMachi 26, 2025, wakati wa ukaguzi wa miradi miwili inayotekelezwa ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo uboreshaji wa barabara za ndani ya hifadhi na upanuzi wa uwanja wa ndege.

“Tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Saadani, sasa endeleeni kusimamia miradi hii ili kuhakikisha inakamilika kwa viwango vya juu na kuleta manufaa kwa sekta ya utalii. Pia, tunashauri uwekezaji zaidi katika miundombinu mingine kama hoteli na huduma za usafiri ndani ya hifadhi ili kuvutia wageni wengi zaidi.” Alisema Mhe. Hasunga.

Aidha, Mhe. Hasunga alipongeza Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Wadhamini TANAPA na Menejimenti ya Shirika kwa kufanikisha ongezeko kubwa la mapato ya hifadhi hiyo, ambapo mapato ya watalii wanaotembelea hifadhi kwa njia ya ndege yameongezeka kufikia shilingi bilioni 1.68 kuanzia Julai hadi Machi mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na makadirio ya ukusanyaji wa kiasi cha shilingi bilioni 1.41 katika kipindi cha miezi 8.

Vilevile, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara, alitoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha fedha za kutekeleza miradi hiyo na kuongeza kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.

“Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika Hifadhi za Taifa inatekelezwa kwa ufanisi. Hatua hii ni muhimu kwa mustakabali wa utalii nchini, na tunapaswa kuendelea kuwekeza zaidi ili kuvutia watalii wengi na kukuza uchumi wa Taifa,” alisema Jenerali Waitara.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Juma Kuji alieleza kuwa maboresho ya miundombinu ya utalii Saadani yameongeza mvuto wa hifadhi kwa watalii, hali inayosaidia kuongeza idadi ya watalii na mapato. Pia, alibainisha kuwa miundombinu bora huongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa watalii hivyo kuimarisha shughuli za utalii.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Afisa Uhifadhi Mkuu Gladys Ng'umbi, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, alieleza kuwa maboresho ya miundombinu hiyo yamezingatia viwango vya kimataifa ili kuhakikisha uwanja wa ndege wa Saadani unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege nyingi na kubwa zaidi.

“Maboresho ya uwanja huu yamezingatia viwango vya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili kuhakikisha kuwa uwanja wa ndege wa Saadani unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba watalii 35 hadi 40 kwa ndege moja ambapo uboreshaji huo utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja kutembelea hifadhi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii”. alisema Ng’umbi.

Hifadhi ya Taifa ya Saadani imekuwa ikifanya maboresho ya miundombinu ya hifadhi ili kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo ni muhimu kiikolojia kwani inakutanisha nyika na bahari katika ukanda wa pwani ya Afrika mashariki.