TAARIFA YA MAFANIKIO YA KIPINDI CHA MIAKA MITATU YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA (2021 – 2024)
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanya wasilisho kwa wahariri wa vyombo vya habari katikamkutano ulioandaliwa na ofisi ya msajili wa hazina jijini Dar es salaam tarehe 21.03.2024. Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA ndugu Juma Nassoro Kuji alieleza kwa lengo la kuongea na wahariri hao lilikuwa ni kuuhabarisha Umma mafanikio yaliyopatikana katika Hifadhi za Taifa katika kipindi cha miaka mitatu (2021 – 2024) ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Msingi wa mafanikio ambayo TANAPA imeyapata ni jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zimeambatana na ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye kukuza sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii ikiwemo ushiriki wake kwenye filamu maarufu ijulikanayo kama “Tanzania: The Royal Tour”. Filamu hii imeleta chachu kubwa katika ukuaji wa utalii nchini.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na;-
A. KUKUZA NA KUENDELEZA SHUGHULI ZA UTALII
Kama nilivyoeleza hapo awali, Filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” ilifungua milango ya utalii na fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa hasa baada ya nchi kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19.
i.) Kuongezeka kwa idadi ya watalii
Katika Hifadhi za Taifa kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa mwaka hadi mwaka. Mfano katika mwaka 2018/2019 jumla ya Watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa walikuwa watalii 1,452,345 ikihusisha watalii wa ndani (719,172) na nje (733,173). Hata hivyo, idadi hiyo ilianza kupungua mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga ya UVIKO-19 na kusababisha idadi ya wageni kupungua hadi kufikia watalii 485,827 katika mwaka 2020/2021. Kufuatia anguko hili la Utalii, Serikali ya awamu ya sita (6) ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum (Standard Operating procedures - SOPs) ya kupokea na kuhudumia watalii, na pia kuruhusu upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19. Hili lilienda sambamba na utangazaji mahiri wa vivutio vyetu kupitia filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa 2022.
Kutokana na jitihada hizo za Mhe. Rais, mnamo mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,873. Hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437. Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 – Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) wametembelea Hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia 5 ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika. Aidha, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).
Vilevile, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024. Ongezeko hili limechangia ongezeko la mapato.
ii.) Kuongezeka kwa Mapato
Katika kipindi cha miaka mitatu, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024) Shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 mpaka Machi 2024. Kiasi hiki (Bilion 340) ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15. Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024.
Mapato haya ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO – 19 ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika.
Ongezeko hili la watalii na mapato linaenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani Bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.
iii.) Kuongezeka kwa masoko mapya ya Utalii
Kumekuwepo na kuchipuka kwa masoko mapya ya utalii yenye idadi kubwa ya watalii ambapo inatoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kuja kutembelea Hifadhi za Taifa. Masoko haya mapya ni pamoja na China, Urusi, Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli.
iv.) Kutambulika Kimataifa
TANAPA imefanikiwa kupata tuzo ijulikanayo kama “Best Practice Award” ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya “European Society for Quality Research - ESQR”. Tuzo hii ya utoaji wa huduma bora kimataifa hutolewa na taasisi hiyo baada ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu kimataifa.
TANAPA imeendelea kupata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne (4) mfululizo ambazo kati ya hizo tuzo za miaka mitatu (3) mfululizo zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha “Platinum category” mwaka 2021, “Gold category” mwaka 2022 na “Diamond category” mwaka 2023.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo itolewayo na shirika la “World Travel Awards (WTA)” ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo (2019 hadi 2023). Tuzo tatu (3) kati ya hizo tano (5) zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita (tuzo za mwaka 2021 hadi 2023).
Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kilimanjaro zilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii (best of the best outdoor enthusiasts). Tuzo hizi hutolewa na jukwaa la kimataifa lijulikanalo kwa jina la “Trip Advisor”. Pia, kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza mwaka huu 2024 imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa namba moja ya Alama za Asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni (World’s topmost unforgettable natural landmarks).
Tuzo hizi zimeliongezea Shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi.
v.) Kuongezeka kwa Uwekezaji wa Malazi
Kumekuwa na ongezeko la maeneo ya malazi na wawekezaji katika Hifadhi za Taifa. Uwekezaji umelenga kuboresha huduma za malazi katika Loji, Kambi za Kudumu (Permanent Tented Camps - PTC), Kambi za Muda (Seasonal Camps), Kambi za Jumuiya (Public Camp Sites), Mabanda (cottages) na Hosteli. Uwekezaji huu umeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 5,755 mwaka 2021 hadi vitanda 10,094 mwaka 2024. Hata hivyo, ujenzi wa malazi unaendelea wenye uwezo wa vitanda 1,148 ambapo ukikamilika kutakuwa na vitanda 11,242.
Kumekuwepo na ongezeko la wawekezaji kwenye maeneo ambayo yaliyokuwa hayana mvuto kwa wawekezaji zikiwemo Hifadhi za Ruaha, Saadani na Mikumi.
Jumla ya maeneo mapya ya uwekezaji 176 (34 ni loji na 142 ni kambi) yameainishwa katika Hifadhi zote kwa kuzingatia mipango ya uendeshaji wa kila Hifadhi na yametangazwa kwenye tovuti ya Shirika.
vi.) Kuongezeka kwa Bidhaa za Utalii
Kumekuwepo na ongezeko la bidhaa za utalii katika maeneo mengine ambayo awali hayakuwa na bidhaa husika:
Kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto (balloon) kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa hifadhi ya Mikumi;
Utalii wa faru (Hifadhi ya Taifa Mkomazi), utalii wa baiskeli (Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha);
Utalii wa michezo na burudani (Hifadhi ya Taifa Serengeti – Mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi – Mpira wa miguu, pete na kikapu).
Ongezeko kwa mbio za Marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa ambapo zimekuwa zikivutia washiriki wengi na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika. Hifadhi zilizofanikiwa kuratibu mbio za Marathoni ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi-Chato na Kilimanjaro.
vii.) Kujiunga na Mfumo wa Utoaji wa Huduma kwa kiwango cha Kimataifa (ISO)
Mwaka 2018 TANAPA iliingia katika mchakato wa kutambuliwa na Shirika la Viwango Duniani ili kujijengea kuaminiwa na wateja. Kutambuliwa kwa TANAPA mwaka 2021 na ISO kumepelekea wateja kuamini na kuchagua huduma zinazotolewa na TANAPA na hifadhi zake hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato. Katika miaka mitatu, Shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja.
viii.) Kuimarishwa kwa Miundombinu ya Ukusanyaji wa Mapato
TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku. Katika kipindi cha miaka mitatu TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika Hifadhi za Taifa Tarangire (2), Mkomazi (3), Serengeti (2) na Nyerere (3).
ix.) Ushindi Katika Uandaaji Bora wa Hesabu
TANAPA imekuwa ikishinda tuzo za uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa kwa upande wa taasisi za umma zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Shirika limekuwa mshindi wa pili wa tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu za mwaka 2022 katika kundi la taasisi za kiserikali zinazotumia mfumo wa IPSASs (2nd winner in the government agencies category (users of IPSASs) for the best presented financial statements award for the year 2022).
x.) Kuimarishwa kwa Miundombinu
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeendelea kuboresha (kujenga na kukarabati) miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa. Shirika lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 mwaka 2024.
Kazi nyingine za miundombinu zilizofanyika ni pamoja na:-
Kukarabati wastani wa kilometa 3,938 za Barabara;
Kutengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334.
Ujenzi wa madaraja 14 na vivuko 399
Kukarabati viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi za Serengeti (1), Nyerere (3), Tarangire (1), Mkomazi (2), Saadani (1), Mikumi (1) na Ruaha (2). Aidha, viwanja vya kutua helikopta (helipads) (5) katika Mlima Kilimanjaro vilijengwa kwa kiwango cha zege kwa kuzingatia kanuni za TCAA na ICAO.
Kununua mitambo 59 ya aina mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Dunia (Mradi wa REGROW) na IMF (Mradi wa TCRP).
Mitambo iliyonunuliwa kupitia mradi wa Mradi wa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth - REGROW) ni motor grader 5, compactor 3, low loader 2, malori 17, excavator 2, bulldozers 2, concrete mixers 5, matrekta 7, malori ya kubebea maji 5, magari ya sinema (cinema vans) 4, magari ya kutolea elimu kwa wanafunzi na jamii “expedition trucks” 3 na malori ya kutengenezea magari (mobile workshop) 5. Jumla ya shilingi 27,873,761,395.00 zilitumika kununua mitambo hiyo.
Mitambo iliyonunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) ni motor grader 5, compactor 4, low loader 4, malori 15, excavator 4, magari madogo 7 (Landcruiser), concrete mixer 1, Back low loader 1 na malori ya kubebea maji 4) vyenye thamani ya shilingi 17,765,532,026 zilitumika kununua mitambo hiyo. Mitambo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi zetu.
B. UTANGAZAJI WA VIVUTIO VYA UTALII KIDIGITALI
Shirika limejikita katika kuboresha mbinu za utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa kwa njia ya kidigitali ili kuwafikia walengwa wengi zaidi na kwa wakati mfupi. Miongoni mwa mikakati ya utangazaji wa vivutio kidigitali ni pamoja na:-
i. Kuongeza Idadi ya Wafuatiliaji Katika Mitandao ya Kijamii
TANAPA imeweza kuongeza wafuatiliaji kwenye mitandao ya kijamii (facebook, Instagram, youtube, tiktok na twitter/X) kutoka watazamaji (viewers) 1,327,000 katika mwaka 2021 hadi kufikia watazamaji 8,960,000 katika mwaka 2024 na wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii ya Shirika (followers) kutoka 62,000 mwaka 2021 hadi wafuatiliaji 1,014,000 mwaka 2024. Hii inaonesha kufuatiliwa kwa shughuli zinazotekelezwa na Hifadhi za Taifa kila siku.
ii. Kuzinduliwa Kwa Usanifu wa Taarifa za Shirika Katika Mfumo wa Kidigitali
Usanifu wa taaarifa za majarida na vipeperushi katika mfumo wa “Quick Reference” (QR Code)” umewezesha upatikanaji wa taarifa za Shirika na hifadhi kwa urahisi, kwa wakati, kwa lugha saba (7) tofauti kwa wakati mmoja (kiswahili, kiingereza, kijerumani, kirusi, kichina, kifaransa na kispaniola) na kupunguza matumizi ya karatasi.
C. USHIRIKISHWAJI JAMII KATIKA UHIFADHI
Katika kipindi cha miaka mitatu, Shirika limeendelea kuboresha mahusiano na jamii zilizo jirani na hifadhi za Taifa katika shughuli za uhifadhi na utalii. Kupitia mashirikiano haya zimepatikana faida mbalimbali ikiwemo:
i. Kuibuliwa na Kutekelezwa kwa Miradi ya Kijamii “Support for Community Initiated Projects” (SCIPs)
Katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya miradi 59 ya kijamii yenye thamani ya shilingi 30,785,819,981 ilitekelezwa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 20, mabweni 2, nyumba 7 pacha za walimu, zahanati 12, nyumba pacha za wauguzi 6, miradi ya maji 6, barabara 5 zenye urefu wa kilomita 76 na bwalo la chakula kwa wanafunzi 1 na ununuzi wa madawati 680. Miradi hii imetekelezwa katika Wilaya za Ruangwa, Makete, Mbeya, Mbarali, Mpanda - Halmashauri ya Nsimbo, Uvinza, Kigoma, Muleba, Bariadi, Bunda, Serengeti, Mbulu, Arumeru, Rombo, Longido, Mwanga, Same, Korogwe, Lushoto, Pangani, Kilosa, Kilombero, Kilolo, Lindi na Ngorongoro (tarafa za Loliondo na Sale). Ujenzi wa miradi hii umesaidia kupunguza kero kwa jamii na kuongeza usalama wa wanafunzi na kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya sambamba na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo. Aidha, miradi hii imesaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na hifadhi na kuifanya jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa Maliasili.
ii. Utekelezwaji wa Miradi ya Uzalishaji Mali (TANAPA Income Generating Projects - TIGPs)
Jumla ya vikundi 138 vimewezeshwa miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji. Jumla ya shilingi billion 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali. Pia, Benki za Kijamii za Uhifadhi “Community Conservation Bank” (COCOBA) 159 zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha shilingi 1,453,272,934. Miradi hii imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa Maliasili.
iii. Kutolewa kwa Ufadhili wa Masomo kwa Wananchi Kupitia Mradi wa REGROW
Jumla ya wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma hapa nchini. Ufadhili huu utasaidia kuongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika.
iv. Kuendelea Kuwezesha Uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na Utoaji wa Hati za Kimila (Community Customary Right of Occupancy - CCRO’s)
TANAPA kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) na Shirika lisilo la kiserikali la “Frankfurt Zoological Society - FZS” imeendelea kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 57 vya wilaya za Serengeti, Morogoro, Kisarawe, Ulanga, Tunduru na Liwale na kutoa hati za kimila 16,243. Kati ya hati hizo, hati 9,874 zilitolewa kwa jamii kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Nyerere na hati 6,612 zilitolewa kwa jamii kutoka kwenye vijiji vilivyo katika wilaya ya Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti. Hata hivyo tunaendelea kuandaa hati za kimila kwenye Wilaya za Bunda, Bariadi, Tarime, Meatu, Itilima na Busega. Uandaaji huu wa matumizi bora ya ardhi unasaidia kupunguza migogoro ya kimatumizi kati ya binadamu na wanyamapori kwenye maeneo husika na kuwajengea usalama katika umiliki wa ardhi kwa jamii zinazopakana na hifadhi.
V.) Kuelimisha Jamii Kuhusu Uhifadhi
Kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wananchi wanaofikiwa na elimu ya uhifadhi kutoka wananchi 169,245 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia wananchi 211,986 katika mwaka wa fedha 2022/2023. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Desemba 2023 wananchi 125,389 wamefikiwa na elimu ya uhifadhi. Ongezeko hili linatoa uhakika wa kuwa na wanajamii wanaoelewa masuala ya uhifadhi na hivyo kuongeza uhakika wa ushiriki wa wananchi kwenye uhifadhi na ulinzi wa maliasili.
Vi). Upandaji wa Miti
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi, Shirika limefungua vitalu na kugawa miche ya miti ya matunda, mbao na vivuli kwa wananchi. Jumla ya miche 209,690 imegawiwa kwa wananchi katika kipindi husika katika hifadhi za Kilimanjaro, Milima ya Udzungwa, Arusha, Serengeti na Burigi-Chato.
D. UTATUZI WA MIGOGORO YA MIPAKA NA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU
i.) Utatuzi wa Migogoro ya Mipaka
Serikali imekamilisha utatuzi wa migogoro minne (4) iliyodumu kwa muda mrefu kati ya vijiji na Hifadhi za Taifa Serengeti (vijiji 7 wilaya ya Serengeti), Arusha (Farm 40/41 - Wilaya ya Arumeru), Tarangire (Kimotorok - Wilaya ya Simanjiro) na Manyara (Buger - Wilaya ya Karatu).
Pia, Serikali inaendelea kutatua migogoro na kufanya uthamini katika Hifadhi za Taifa za Ruaha (Ihefu), Milima ya Mahale (Vitongoji vya Kabukuyungu na Mahasa Kijiji cha Kalilani), Saadani (Kitongoji cha Uvinje), Mkomazi (Kitongoji cha Kimuni), Arusha (Kijiji cha Nasula) na Kitulo (Wilaya ya Rungwe).
Jumla ya vigingi 905 vimejengwa katika Hifadhi za Taifa za Serengeti (184), Ruaha (671), Ziwa Manyara (18) na Tarangire (32) pamoja na kulima MKUZA wenye urefu wa kilometa 609 (Tarangire - 242, Ruaha - 344 na Mikumi - 23) kufuatia utatuzi wa migogoro iliyokuwepo.
Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wa vijiji vya Nyatwali, Serengeti na Tamau ili kutwaa eneo la Ghuba ya Speke kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
ii.) Kukabiliana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu
Shirika limeendelea kukabiliana na kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu. Katika kipindi hiki, Shirika limeshughulikia kwa wakati matukio 4,954 yaliyoripotiwa. Pia, Shirika limeweza kufunga visimbuzi (Global Positioning System - GPS collar) kwa makundi 12 ya tembo, makundi 12 ya simba na makundi 5 ya mbwa mwitu katika hifadhi za Mkomazi, Serengeti, Mikumi, Nyerere na Ruaha. Ufungaji huu wa visimbuzi kwa makundi hayo ya wanyama unasaidia ufuatiliaji wa karibu kwa makundi husika na kuweza kutambua mienendo yao ili kurahisisha udhibiti wanapotoka nje ya maeneo ya hifadhi.
Vilevile, kupitia mradi wa REGROW, Shirika limewezesha mafunzo kwa askari wa vijiji (Village Game Scout – VGS) 354 kutoka vijiji 39 ili kuwezesha kukabili kwa wakati matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, Shirika linaendelea na ujenzi wa vituo 8 vya Askari Uhifadhi katika maeneo ya kimkakati yaliyopo katika vijiji vinavyoathirika zaidi katika wilaya za Mbarali, Kalambo, Kilwa, Namtumbo, Ruangwa, Serengeti, Bunda na Bariadi. Vituo hivi vitasaidia askari kudhibiti kwa wakati wanyamapori wakali na waharibifu.
E. KUKUA KWA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA SHIRIKA
Shirika limeendelea kujikita katika matumizi ya teknolojia mbalimbali ambayo yamesaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kila siku. Matumizi ya teknolojia hizi ni pamoja na:-
i. Kuimarishwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kidigitali kwa kuanzisha “online reservation and booking system”;
ii. Mfumo wa kufanya malipo ya vibali vya kuingia hifadhini yaani “e-permit” ambao unamuwezesha mtalii kufanya malipo akiwa sehemu yoyote ile duniani kabla hajaingia hifadhini;
iii. Kuanzisha matumizi ya “smart gates” katika malango 8 (Serengeti - 4, Tarangire - 3 na Ziwa Manyara - 1) ili kuongeza udhibiti wa mapato;
iv. Kuanzishwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wateja kuhusu utoaji wa huduma (online customer feedback);
v. Kuimarishwa kwa ulinzi wa wanyamapori kupitia teknolojia ya "Low Range Wide Area Network" (LoRa WAN) yenye uwezo wa kuona eneo kubwa la hifadhi;
vi. Kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya taarifa za kijiografia. Mifumo hii inasaidia kuongeza ufanisi katika doria za kuzuia ujangili;
vii. Kuongeza matumizi ya ndege nyuki (drones) kwenye kuimarisha ukaguzi wa maeneo ya Hifadhi za Taifa. Matumizi haya yameongeza tija kwa kuwezesha ukaguzi wa maeneo makubwa ndani ya muda mfupi; na
viii. Kuendeleza matumizi ya ndege kwenye doria za kukabiliana na uvunaji haramu wa maliasili ndani ya Hifadhi.
F. UANZISHWAJI WA VYANZO BUNIFU VYA MAPATO
Shirika limeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa linabuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vitaliingizia Shirika fedha na kuongeza ukusanyaji wa mapato. Miongoni mwa vyanzo bunifu vya mapato ambavyo vimeendelea kuibuliwa na Shirika ni pamoja na;-
i. Kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika (TANAPA Investment Limited – TIL) inayolenga kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na pia kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Shirika kwa kutekeleza miradi mbalimbali;
ii. Kuanzishwa kwa Kiwanda cha Ushonaji wa sare za watumishi na kupokea zabuni kutoka taasisi nyingine;
iii. Ujenzi wa Hoteli yenye hadhi ya nyota tatu katika eneo la Rubambagwe Wilaya ya Chato yenye vyumba 30 vya kulala; na
iv. Ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa hadhi ya kimataifa wenye mashimo 18 uliopo eneo la Forti Ikoma - Hifadhi ya Taifa Serengeti.
G. KUIMARIKA KWA UHIFADHI WA WANYAMAPORI WALIO HATARINI KUTOWEKA
Shirika limeendela kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka na kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya Wanyama hao wakiwemo faru, mbwa mwitu na sokwe.
H. KUDHIBITI UVUNAJI WA MALIASILI
Jukumu la msingi la Shirika ni kusimamia maliasili zote zilizopo katika hifadhi za Taifa hapa nchini pamoja na usalama wa watalii na wawekezaji waliopo katika maeneo yanayosimamiwa na Shirika. Serikali ya awamu ya sita (6) imeweka mazingira wezeshi kwa Shirika kusimamia maliasili zilizopo katika Hifadhi za Taifa hapa nchini. Mazingira wezeshi ni pamoja na upatikanaji wa rasimilimali fedha, rasilimali watu na vitendea kazi kama magari, mitambo ya kutengeneza barabara na mafunzo kwa watendaji. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
i. Kudhibiti uwindaji wa wanyama adimu ambapo hakukuwa na tukio la kuuawa kwa Faru, Sokwe au Mbwa mwitu.
ii. Kupungua kwa matukio ya uwindaji wa tembo kutoka matukio 4 kwa mwaka 2021/2022 hadi matukio mawili (2) kufikia Machi 2024.
iii. Kukamata silaha mbalimbali 274 (shot gun 13, Assault Riffles-7 (SMG, SAR na AK 47), Riffle – 7 (.458, .404, .375, 30-06), magobore 245 pamoja na kutegua nyaya 48,665.
iv. Kudhibiti uingizwaji wa mifugo hifadhini kwa kufanya doria na kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazoishi jirani na hifadhi. Madhara ya uingizaji wa mifugo ni pamoja na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji, maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama wafugwao kwenda kwa wanyamapori, kuendelea kushamiri na kusambaa kwa mimea vamizi na kuharibu shughuli za utalii.
v. Kusimamia na kuendesha mashauri katika mahakama mbalimbali hapa nchini dhidi ya wahalifu waliokamatwa. Jumla ya mashauri 4,831 yalitolewa maamuzi kati ya mashauri 4,978 yalifunguliwa na kusikilizwa.
I. MAFANIKIO MENGINEYO
Shirika limeendelea kuajiri, kutoa mafunzo na kutoa motisha mbalimbali kwa watumishi wake ili kuongeza ufanisi, ubunifu na tija katika shughuli za uhifadhi na utalii. Shirika limefanikiwa kuongeza idadi ya watumishi kutoka watumishi 2,969 mwaka 2021 hadi kufikia watumishi 3,104 Machi, 2024. Aidha, Shirika linakamilisha taratibu za kuajiri watumishi wengine 220. Ongezeko la idadi ya watumishi linachangia kuongeza ufanisi katika usimamizi na uendeshaji wa Hifadhi za Taifa.
J. CHANGAMOTO
Shirika linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo: -
i. Mabadiliko ya tabia nchi; (ukame, mafuriko n.k)
ii. Uwepo wa mimea vamizi inayoathiri upatikanaji wa chakula na mizinguko ya wanyamapori;
iii. Uwepo wa ujangili;
iv. Matukio ya uingizwaji wa mifugo ndani ya hifadhi;
v. Matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya jamii;
vi. Gharama kubwa za matengenezo ya miundombinu ya barabara kutokana na mvua nyingi (el-nino); na
vii. Uchache wa miundombinu nje na ndani ya hifadhi za kusini, mashariki na magharibi mwa nchi unaosababisha wawekezaji wachache.
K. MIKAKATI YA JUMLA YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO
Shirika limeendelea kujiimarisha katika jitihada za utatuzi wa changamoto zinazolikabili. Miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa kama sehemu ya kukabiliana na baadhi changamoto zilizopo za uhifadhi na utalii ni pamoja na:-
i. Kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii;
ii. Kuelimisha jamii kuhusu mbinu za awali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwa wanasubiri msaada zaidi kutoka kwa Askari wa Uhifadhi na pia kuwapatia vifaa vya kujikinga kama vile mabomu ya pilipili, vuvuzela, tochi nk;
iii. Kuendelea kushauri jamii kuheshimu maeneo ya mapito ya wanyamapori ili kupunguza migongano kati ya wanyamapori na wananchi;
iv. Kuendelea kutangaza vivutio vya utalii katika masoko mapya yanayoibukia kama vile Israeli, Brazili, Jamhuri ya Czech, Urusi, Jamhuri ya Watu wa China, India na Afrika ya Kusini;
v. Kutumia teknolojia katika kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii;
vi. Kutumia matokeo ya tafiti kuwezesha kufanya maamuzi ya namna ya kusimamia maliasili;
vii. Kuhamasisha na kutoa motisha kwa wawekezaji kuwekeza katika hifadhi za kusini, mashariki na magharibi mwa nchi ambako kutaleta mtawanyiko wa wageni;
viii. Kushirikiana na wadau mbalimbali kutangaza utalii ndani na nje ya nchi zikiwemo Ofisi za Balozi, hoteli, waongoza watalii na kampuni za utalii;
ix. Kuimarisha utendaji kazi kwa mfumo wa kijeshi ili kutoa fursa kwa watumishi kuwa na nidhamu stahiki, ukakamavu na utayari wakati wote kutekeleza majukumu yao kwa ari, ufanisi, uzalendo na weledi.
x. Kutatua migogoro iliyopo kati ya Hifadhi za Taifa na jamii na kuzuia migogoro mipya.
xi. Kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kutumia tabaka gumu katika barabara zinazopitisha idadi kubwa ya magari hususan katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania litataendelea kusimamia jukumu la kuhifadhi maliasili zote na kutunzwa kikamilifu wakati wote. Ulinzi wa malisili, usalama wa watalii, usalama wa watumishi wa TANAPA, na usalama wa wawekezaji utaendelea kuimarishwa wakati wote ili kuhakikisha kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania zinaendelea kuwa ni maeneo salama na sahihi kwa watalii na wawekezaji.
Kamishna Kuji alitoa wito wa kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo yaliyoainishwa katika Hifadhi za Taifa kwa nia ya kuboresha huduma za malazi kwa wageni. Sambamba na uwekezaji, Kamishina Kuji alitoa wito kwa watanzania kutembelea hifadhi zetu kwa ajili ya kujivinjari na kupumzika.