WAZIRI KIKWETE : MWENGE WA UHURU NI TUNU NA ISHARA YA UTAIFA WETU.
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, jana Oktoba 15, 2024 amepokea Mwenge wa Uhuru na kuukabidhi kwa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa ajili ya kuupandisha katika kilele cha mlima Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa mbio za Mwenge huo na kusisitiza kuwa Mwenge wa uhuru ni tunu na ishara ya utaifa wa Taifa letu.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Kikwete alisema kuwa mwenge wa uhuru kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifa letu uliwashwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Disemba 1961, akitekeleza kwa vitendo maneno yake ya kifalsafa aliyoyatamka katika baraza la kikoloni la kutunga sheria (Tanganyika Legislative law) mwaka 1958 kuwa Mwenge ukatoe mwanga kupambania uhuru wa nchi za Afrika, kwani aliamini kupata uhuru kwa njia ya maridhiano ni bora zaidi kuliko kwa mtutu wa bunduki.
Waziri Kikwete aliongeza, “Wakati wa harakati za kutangaza uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliwasha Mwenge huo na kumkabidhi Luteni Alexander Nyirenda na wenzake kuupandisha katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa na ishara ya matumaini na amani kwa watu waliokata tamaa hususani kwa nchi ambazo zilikuwa bado ziko chini ya himaya za wakoloni”.
Vilevile, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya hivi akiamini kuwa mlima huu ambao ni mrefu kuliko milima yote barani Afrika na mlima wa pili kwa urefu duniani ni sehemu sahihi ya kufikisha ndoto na maono yake kwa Watanganyika, Waafrika na wananchi wa mabara mengine waliokuwa wakikabiliwa na madhira ya ukoloni Mamboleo, alisema Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete aliongeza kuwa wakati Mwl. J.K. Nyerere akiuwasha Mwenge huu tunaoupandisha leo alinukuliwa akisema, "Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu ulete matumaini pale ambapo hamna tumaini na ulete upendo penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau" na hii falsafa ya mwenge wa uhuru ndiyo fungate lilipo kati ya Mwenge huu na Mlima Kilimanjaro”.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro hivyo kupelekea hifadhi hiyo kupendekezwa kupigiwa kura kwa ajili ya kuwa kivutio bora barani Afrika na Duniani.
"Nitumie fursa hii kuwahamasisha Watanzania kupigia kura Mlima Kilimanjaro ili uweze kushinda tuzo hiyo na kuwavutia wageni wengi zaidi" aliongeza Waziri Pindi.
Aidha, Waziri Ridhiwani alimshukuru Mhe. Pindi Chana, Menejimenti na watendaji wote wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) hususani KINAPA kwa kuratibu vizuri jambo hili ambalo kimsingi utekelezaji wake unaanza leo hadi hapo Mwenge na bendera vitakapofikishwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro na makamanda hao watakaporejea salama salmini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, watendaji wa taasisi za Serikali, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na viongozi wa dini.