𝐊𝐀𝐌𝐈𝐒𝐇𝐍𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐈: 𝐌𝐀𝐀𝐅𝐈𝐒𝐀 𝐍𝐀 𝐀𝐒𝐊𝐀𝐑𝐈 𝐖𝐀 𝐇𝐈𝐅𝐀𝐃𝐇𝐈 𝐘𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐁𝐔𝐑𝐈𝐆𝐈 - 𝐂𝐇𝐀𝐓𝐎 𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐄𝐍𝐈 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐒𝐇𝐔𝐆𝐇𝐔𝐋𝐈 𝐙𝐀 𝐔𝐇𝐈𝐅𝐀𝐃𝐇𝐈 𝐍𝐀 𝐔𝐓𝐀𝐋𝐈𝐈

Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, amehimiza maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato kuwajibika kikamilifu katika kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii.
Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Machi 16, 2025 alipofanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazotekelezwa katika Hifadhi hiyo ambapo alipokelewa na wenyeji wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Mgana Msindai - Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Magharibi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Simon Aweda - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato.
“Ongezeni ubunifu katika utendaji kazi ili kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufikisha idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 za kimarekani kwa mwaka wa fedha mwaka 2025” alisema Kamishna Kuji.
Hali kadhalika, Kamishna Kuji alisisitiza kutumia rasilimali watu vizuri pamoja na kuruhusu ubunifu wenye tija katika utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Simon Aweda alimshukuru Kamishna Kuji kwa kutenga muda wake na kukutana na watumishi. Kamishna Aweda alieleza kuwa hifadhi inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo ipo mpaka mwa nchi ambazo ni Rwanda, Burundi na Uganda.
“Hifadhi yetu inazidi kuimarika kiusalama na ina nafasi kubwa ya kukua kiutalii kwani kuna fursa mbalimbali za uwekezaji wa kambi za watalii na hoteli hivyo tunaendelea kutangaza fursa hizi ili kuongeza mapato ya serikali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa” aliongeza Kamishna Aweda.
Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato iliyopo Kanda ya magharibi ni maarufu zaidi kwa wanyama adimu aina ya Mbega Wekundu “Ashy Red Colobus Monkey”.