HIFADHI YA TAIFA RUAHA YAADHIMISHA MIAKA 60 TOKEA KUANZISHWA KWAKE.

Posted On: Oct, 09 2024
News Images

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Hifadhi ya Taifa Ruaha tangu kuanzishwa kwake imepata mafanikio lukuki ikiwemo ongezeko la idadi ya watalii kutoka watalii kutoka watalii 9,657 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia watalii 19,332 kwa mwaka 2023/2024.

Waziri Chana ametoa kauli hiyo leo Oktoba 7, 2024 ikiwa ni Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Ruaha yaliyofanyika katika eneo la Msembe ndani ya hifadhi hiyo ambapo amesema Watalii wameongezeka kwa asilimia mia.

“Mafanikio haya ya Utalii, kwa sehemu kubwa yamechangiwa na jitihada zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutangaza utalii na vivutio vyetu kupitia filamu maarufu zaidi nchini ya “Tanzania: The Royal Tour” pamoja na filamu ya “The Amazing TANZANIA” amesisitiza Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa kufuatia jitihada za Rais Samia, katika mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya watalii wa kimataifa nchini imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,808,205 Mwaka 2023.

Akizungumzia uboreshaji wa miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mhe. Chana amesema Serikali kupitia Mradi wa REGROW iko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wa viwanja viwili vya ndege katika hadhi ya juu kabisa na vya kisasa katika maeneo la Ukwaheri Kusini mwa hifadhi na Msembe yalipo Makao Makuu ya Hifadhi.

Amesema uboreshaji wa miundombinu inayoendelea ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha itasaidia zaidi ya wageni 220 kuweza kuhudumiwa kwa pamoja ikiwa ni wastani wa wageni 140 uwanja wa Kiganga (Msembe) na wageni 80 uwanja wa Ukwaheri.

“Miradi hii itakuwa kichocheo cha ajira katika sekta rasmi na ile isiyo rasmi na hivyo kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha mwananchi wa kawaida katika ngazi ya kaya”amesisitiza.

Aidha, Waziri Chana amesema Serikali kupitia mradi wa REGROW imewezesha jumla ya vijana 218 kufadhiliwa kutoka wilaya za Iringa, Mbarali na Chamwino na jumla ya shilingi za kitanzania 685,164,760 zimetumika kusomesha vijana wenye sifa kutoka katika vijiji vilivyo pembezoni mwa hifadhi hiyo.

Pia, amesema mradi wa REGROW umeendelea kufadhili vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali kupitia mfumo wa COCOBA ambapo jumla ya vikundi 188 vimeanzishwa na vinaendelea kunufaika.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Chana ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa utalii kuwekeza katika maeneo ya hifadhi ya Taifa Ruaha hususan kwenye eneo la huduma za malazi, usafirishaji na utalii kwa ujumla ambapo kwa sasa, Hifadhi ya Taifa Ruaha imetenga maeneo 30 kwa ajili ya uwekezaji wa Malazi ya wageni.

Hifadhi ya Taifa Ruaha ni hifadhi ya nne kuanzishwa baada ya Hifadhi za Taifa za Serengeti (1951), Ziwa Manyara (1960) na Arusha (1960) na ilianzishwa mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na. 464